Wanajeshi wa Kenya kusalia Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekariri kuwa wanajeshi wa Kenya watasalia nchini Somalia, kupambana na wapiganaji wa Kiislamu wa Al shabaab, na kuupuuza ripoti kuwa kenya inapania kuondoa wanajeshi wake ili kuzuia mashambulio zaidi.

Akiongea wakati alipowatembelea wanajeshi waliojeruhiwa wakati wa mashambulio yaliyotekelezwa na Al shabaab katika eneo la Lamu Pwani ya Kenya, rais Kenyatta alisema nia yao kubwa ni kulikandamiza kundi hilo kabisa.

Kenya ilituma wanajeshi wake nchini Somalia mwaka wa 2011 kutokomeza kundi hilo lenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda.

Kwa sasa jeshi la Kenya linahudumu chini ya jeshi la muungano wa afrika AMISOM, ambalo linaunga mkono serikali ya sasa ya somalia.

Wapiganaji wa Al shabaab wameimarisha operesheni zao nchini Kenya, na hivyo kuwa pigo kubwa kwa mipango ya Kenya ya kuwatuma wanajeshi wake katika maeneo ya mipakani kuzuia wapiganaji wa kundi hilo kuingia nchini Kenya.

Rais Kenyatta ambaye alifanya mazungumzo na viongozi wa serikali wanaochangia wanajeshi nchini Somalia ikiwa ni pamoja na viongozi wa mataifa ya Burundi, Djibouti, Ethiopia na Kenya amesema jukumu la Kenya katika vita hivyo ni wazi.

Image caption Alshabaab

Wapiganaji hao wa Al shabaab licha ya kusakwa na wanajeshi hao wa muungano wa Afrika na wanajeshi wa ndege zizizokuwa na rubani za Marekani, nchini Somalia, wamefanikiwa kuwakwepa wanajeshi hao na kuingia nchini Kenya kufanya mashambulio.

Wiki iliyopita wanajeshi wa Kenya walitibua jaribio la wapiganaji hao kufanya mashambulio eneo la Lamu, na kuwauwa wapiganaji kumi na tano.