Mkopo kuimarisha shilingi ya Tanzania

Image caption Sarufi ya Tanzania

Serikali ya Tanzania inatarajia kukopa kiasi cha dola milioni mia nane za Kimarekani kutoka taasisi mbili za kifedha za kigeni ili kuimarisha shilingi ya Tanzania ambayo inaendelea kudorora.

Tayari Tanzania imefanya mazungumzo na taasisi hizo mbili ,Rand Merchant Bank ya Afrika Kusini pamoja na Benki ya Maendeleo ya China.

Benki kuu ina matumaini kwamba fedha hizo ambazo serikali ina mpango wa kukopa kwa ajili ya bajeti yake zitasaidia kuimarisha shilingi.

Katika kipindi cha miezi sita tu, tayari shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 21 na kuwa kati ya sarafu inayofanya vibaya zaidi barani Afrika.

Mkurugenzi wa utafiti wa uchumi na sera Dr Joseph Masawe ameiambia BBC kwamba hata kama lengo kuu la ukopaji wa fedha hizo halikuwa kuimarisha shilingi, upatikanaji wake katika mzunguko wa fedha utasaidia kuiimarisha shilinigi.

"Swala la kukopa pesa nje si geni. Karibu kila mwaka serikali hukopa pesa nje na nia kubwa si kuimarisha shilingi lakini ni kwa ajili ya kutekeleza bajeti yake" amesema Dr Masawe

Dr Masawe amesema sababu za mporomoko ya shilingi ni lazima ziangaliwe kwa mapana na kwamba sababu nyingine zipo nje ya uwezo wa taasisi yake na serikali ya Tanzania.

Amezitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na kuimarika kwa uchumi wa Marekani ambapo umechangia karibu asilimia 65 ya mporomoko huo wakati sababu zingine ni kama vile uchaguzi ujao na uingizwaji wa bidhaa nyingi kutoka nje mambo ambayo hayaepukiki

Wiki iliyopita Waziri wa Fedha wa Tanzania Saada Mkuya aliliambia bunge kuwa serikali ina mpango wa kupunguza utegemezi katika bajeti yake kutoka kwa nchi wahisani kwa asilimia 6.4 katika mwaka huu wa fedha.

Hata hivyo mkakati huo umetiliwa shaka na wachambuzi wanahofu kwamba unaweza kuongeza deni la taifa ambalo hadi mwezi wanne mwaka huu lilifikia takribani dola bilioni 18.9