Madada 3 wa Bradford waliingia Syria

Image caption Madada watatu wa mjini Bradford walioelekea Syria

Madada watatu kutoka mjini Bradford nchini Uingereza na watoto wao tisa wanaohofiwa kusafiri kuelekea nchini Syria wamevuka mpaka ,mfanyibiashara mmoja wa kusafirisha bidhaa kwa njia ya magendo mpakani ameiambia BBC.

Mfanyibiashara huyo wa kundi la Islamic State ambaye anasimamia mipaka inayodhibitiwa na kundi hilo amesema kuwa familia hizo ziligawanywa katika makundi mawili ili kuvuka mpaka na kuingia Syria.

Amesema kuwa kundi la kwanza lilivuka mpaka mapema siku ya jumatano na la pili likaelekea siku ya Alhamisi.

Madada hao Khadija,Sugra na Zohra Dawood pamoja na watoto wao tisa walitoweka baada ya kusafiri nchini Saudia.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ramani ya Syria

Siku ya Jumanne,waume zao walitoa ombi wakiwataka wake zao kurudi nyumbani.

Mwandishi wa BBC Paul Wood,ambaye yuko katika mpaka wa Uturuki na Syria amesema kuwa alizungumza na mfanyibiashara huyo ambaye alithibitisha kuvuka kwa madada hao.

Amesema kuwa habari hizo zinaingiliana na taarifa kwamba mmoja ya madada hao Zohra alituma ujumbe kwa njia ya simu kwa familia yake na kusema kwamba alikuwa nchini Syria,lakini hakusema ni wapi haswa alipo.