Puff Daddy akamatwa kwa shambulizi

Image caption Puff Dadddy

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za Hip hop P Diddy amekamatwa kwa kushukiwa kumshambulia mtu kwa silaha mjini Los Angeles.

Kisa hicho kinadaiwa kufanyika katika chuo kikuu cha California Jumatatu alasiri, mahala ambapo mwanawe wa kiume ni mmojawapo ya wachezaji katika timu ya soka ya Marekani.

Hayo ni kwa mjibu wa maafisa wa polisi.

Silaha hiyo ni kifaa cha chuma kilichoundwa kama mpira, ambacho kinajulikana kama kettlebell, na ambacho hutumika katika mafunzo ya unyanyuaji mizani.

Rekodi za jela zinaonyesha kuwa bwana Diddy ambaye jina lake kamili ni Sean Combs, aliachiliwa huru kwa dhamana ya dola elfu mia moja na sitini, mnamo Jumatatu jioni.

Maafisa bado hawajamtambua mhathiriwa aliyeshambuliwa ama kusema kilichosababisha shambulio hilo.

Mwanawe Combs, Justin Combs, alikuwa chuoni humo wakati wa tukio hilo.

Justin, amechezea timu ya soka ya Marekani UCLA, mechi kadhaa tangu ajiunge na chuo hicho yapata miaka mitatu iliyopita.

Mwanawe Snoop Dogg, Cordell Broadus pia anaichezea timu hiyo.