2 wauawa siku 1 kabla ya uchaguzi Burundi

Haki miliki ya picha AFP GETTY
Image caption Walioshuhudia mauaji hayo wanawalaumu polisi kwa mashambulizi na vifo hivyo

Watu 2 wameuawa Burundi katika mashambulizi ya gruneti na ufyatulianaji risasi katika ngome za upinzani katika mji mkuu wa Bujumbura siku moja kabla ya uchaguzi wa wabunge.

Uchaguzi huo ambao umekumbwa na utata baada ya makundi ya upinzani kuandamana na ilikupinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.

Upinzani unadai kuwa rais Nkurunziza anakiuka katiba ya taifa na mapatano ya Arusha yalyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Walioshuhudia mauaji hayo wanawalaumu polisi kwa mashambulizi na vifo hivyo vilivyotokea katika maeneo ya mji mkuu wa Bujumbura ambayo yanadhaniwa kuwa ni ngome ya vyama vya upinzani.

Jumamosi watu waliokuwa wamejihami na bunduki walivamia kituo cha kuhifadhia makaratasi ya kupigia kura na kuyachoma moto.

Haki miliki ya picha
Image caption Upinzani umekuwa ukiandaa maandamano mjini Bujumbura ilikumshinikiza Nkurunziza ajiondoe katika kinyang'anyiro cha urais

Tukio hilo lililotokea Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo iliwaacha wengi vinywa wazi wasijue waliotekeleza mashambulizi hayo ni kina nani wala nia yao ilikuwa nini.

Burundi imekumbwa na mzozo wa kisaisa tangu rais Nkurunziza atangaze nia ya kuwania muhula wa tatu.

Upinzani umekuwa ukiandaa maandamano mjini Bujumbura ilikumshinikiza ajiondoe katika kinyang'anyiro hicho.

Haki miliki ya picha
Image caption Rais Nkurunziza amekataa kuahirisha uchaguzi

Rais Nkurunziza amekataa kujiondoa akisema kuwa muhula wa kwanza aliohudumu kama rais alikuwa amechaguliwa na wawakilishi wa wajumbe wala sio uma kama inayohitajika katika katiba.

Vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali tayari yametangaza kuwa watasusia uchaguzi huo.

Bwana Nkurunziza alichaguliwa kuingoza nchi hiyo na wajumbe katika mkutano wa amani wa Arusha uliokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Takriban watu 50 wameuawa nchini Burundi tangu mwezi Aprili mwaka huu wakati rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kuwa atawania muhula wa tatu.

Image caption Raia 100,000 wa Burundi nao wamekimbilia mataifa jirani kwa hofu ya kuzuka mamchafuko zaidi.

Raia wengine 100,000 wa Burundi nao wamekimbilia mataifa jirani kwa hofu ya kuzuka mamchafuko zaidi.

Uchaguzi wa ubunge unatarajiwa siku ya Jumatatu huku uchaguzi wa urais ukipangiwa kufanyika tarehe 15 Julai mwaka huu.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki moon alikuwa ametoa ombi uchaguzi huo uahirishwe kutokana na hali ya taharuki iliyotanda nchini humo.