Benki nchini Ugiriki kuendelea kufungwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bendera kutoka kulia:bendera ya Ugiriki, Benki ya Taifa ya Ugiriki na bendera ya Umoja wa Ulaya, EU zikipepea mbele ya makao makuu ya Benki ya Taifa

Waziri mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras amesema benki za nchi hiyo na masoko ya hisa yataendelea kufungwa na kudhibiti mitaji.

Katika hotuba yake aliyoitoa kupitia televisheni, Bwana Tsipras ameomba kuwepo na utulivu, hakusema kufungwa kwa shughuli za kibenki kutadumu hadi lini, lakini amewahakikishia watu kuwa akiba zao, mishahara na malipo ya pensheni ni salama.

Bwana Tsipras ameishutumu Benki Kuu ya Ulaya, ECB, kwa ulaghai juu ya uamuzi wake wa kutotoa fedha za dharura kwa Ugiriki.

Hatua ya ECB inafuatia kuvunjika kwa mazungumzo ya Jumamosi kati ya Ugiriki na nchi zinazotumia sarafu ya Euro juu ya makubaliano ya kuinusuru Ugiriki kutokana na madeni yake yaliyopewa muda wa utekelezaji kufikia Jumanne.