Ombi la Ugiriki lakataliwa

Haki miliki ya picha .
Image caption Alexis Tsipras waziri mkuu wa Ugiriki

Mawaziri wa nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya euro wamekataa ombi la serikali ya Ugiriki la kutaka kuongezewa muda wa kunusuru uchumi wake, saa chache kabla ya kumalizika kwa muda wa kulipa deni lake kwa Shirika la Fedha Duniani, IMF, la euro bilioni 1.6.

Hatua hiyo imekuja baada ya mawaziri kufanya mkutano wa dharura kwa njia ya simu.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras alikuwa ametoa ombi la kutaka kuongezewa muda wa miaka miwili wa kunusuru uchumi.

Iwapo itashindwa kulipa deni lake kwa IMF, Ugiriki iko katika hatari ya kuondolewa katika umoja wa nchi za Ulaya zinazotumia sarafu ya euro.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu wa Ugiriki Yannis Dragasakis, Ugiriki pia iliiomba IMF kupewa muda zaidi wa kulipa deni lake. Mwenyekiti wa nchi za kundi la Euro na ambaye pia ni waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem amesema haitawezekana kuiongezea Ugiriki muda wa kulipa deni lake zaidi ya muda uliokuwa umepangwa huku nchi hiyo ikikataa kukubaliana na mapendekezo ya Ulaya yaliyokuwa yamewasilishwa.

Akizungumza baada ya mkutano amesema ombi la Ugiriki na kupewa msaada mpya wa euro bilioni 29.1 kupitia mpango wa misaada wa Ulaya utafikiriwa baadaye.

Tume ya Ulaya moja ya wakopeshaji wa Ugiriki pamoja na IMF na Benki Kuu ya nchi za euro, wanataka Ugiriki kupandisha kodi na kupunguza matumizi ya ustawi wa jamii ili kutekeleza majukumu yake katika kulipa deni.

Huku kukiwa na wasiwasi kwa Ugiriki kushindwa kulipa deni lake kubwa la euro bilioni 323 na uwezekano wa kutoka katika umoja wa nchi zinazotumia sarafu ya euro - misururu mirefu ya watu inaendelea katika mashine za kutolea fedha nchini Ugiriki, ambapo kiwango cha juu kinachoruhusiwa kutolewa kwa siku ni euro 60.

Benki za Ugiriki hazikufunguliwa wiki hii baada ya mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake kuvunjika. Hata hivyo, matawi 1,000 ya benki yatafunguliwa tena Jumatano ili kuwawezesha watu wa malipo ya pensheni kuchukua fedha yao, kwani wengi wao hawatumii kadi za benki.