Ruto:Kenya haitaruhusu ndoa za jinsia moja

Image caption Naibu rais wa Kenya ameonya kuwa taifa lake halitaruhusu ndoa za jinsia moja

Naibu rais wa Kenya ameonya kuwa ndoa za jinsia moja ni haramu na kuwa hazitawahi kuruhusiwa nchini humo.

Ruto amechukua msimamo huo mkali siku chache tu kabla ya ziara ya rais wa Marekani Barrack Obama nchini Kenya.

Mahakama ya juu nchini Marekani majuzi ilihalalisha ndoa za jinsia moja kote nchini humo.

''kwa kweli uhusiano na ndoa ya jinsia moja kwa hakika inakiuka mpango wa mwenyezi mungu,

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rais wa Marekani Barrack Obama anatarajiwa kuzuru Kenya mwezi huu.

''Mungu hakuwaumba mwanaume na mwanamke ili mwanaume amuoe mwanaume mwenzake wala mwanamke amuoe mwanamke mwenzake'' alisema bwana Ruto alipowahutubia waumini wa kanisa moja jijini Nairobi.

''Tumesikia majuzi wamarekani wamehalalisha ndoa ya jinsia moja na mambo hayo machafu .

''Nataka niwahakikishie kama kiongozi mkristo kuwa mimi ninapinga uchafu huo na nitailinda Kenya,Nitasimamia ukweli na mafundisho ya dini yangu ''

Aliwataka wakristo na Waislamu waungane kupinga shinikizo la aina yeyote ya kuhalalisho ndoa ya jinsia moja nchini Kenya.

''Hata wajaribu vipi ama watumie ushawishi wa nadharia hatutabadilisha msimamo wetu ''

Image caption Viongozi hao hawamtaki Obama aishinikize Kenya kuwatambua wapenzi wa jinsia Moja

''Tunamuamini mwenyezi mungu, na hili ni taifa linalomtukuza Mungu na litaendelea kufanya hivyo''alisema bwana Ruto

Tayari muungano wa viongozi wa madhehebu mbalimbali nchini Kenya chini ya muavuli wa shirika la haki la Wakatholiki na vuguvugu la Wakristu wameaandamana mjini Nairobi wakipinga mapenzi ya jinsia moja.

Wakiungana na wabunge kadhaa waandamanaji hao wamemuonya Obama kuwa watamzomea endapo atajaribu kuishinikiza serikali ya Kenya kuruhusu ndoa ya jinsia moja.

Waandamanaji hao waliokuwa wakiimba ''tunataka ndoa kama ya Obama na Mitchell wala sio Obama na Obama'' walizunguka katikati ya jiji la Nairobi hadi kwenye mahakama kuu ya Kenya na afisi za Mwanasheria mkuu wa Kenya.

Tayari ikulu ya rais imeshatangaza kuwa Obama atakuwa huru kuzungumzia lolote atakapowasili nchini Kenya baadaye mwezi huu.

Image caption Marekani majuzi ilihalalisha ndoa za jinsia moja kote nchini humo

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Obama kuzuru Kenya,nchi alikotoka babake tangu achaguliwe kama rais wa kwanza Marekani mwenye asili ya Kiafrika.

Waandamanaji hao wamesema kuwa wao wanaheshimu uhuru na haki za wamerekani, ambao wamehalalisha ndoa kama hiyo, na kusema kuwa wao kamwe hawataruhusu hayo nchini Kenya.

Sasa wanamtaka rais wa Marekani kutozungumzia lolote kuhusia na suala hilo wakati wa ziara yake nchini Kenya baadaye mwezi huu,

na wameapa kuwa watavuruga shughuli wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu ujasiri mali, ambao rais Obama anatarajiwa kulifungua wakati wa ziara yake ikiwa ataghusia suala hilo.