Mawaziri wa zamani Tanzania wafungwa

Image caption Serikali ilipata hasara ya shilingi bilioni 11. 7

Ni kesi iliodumu takribani miaka saba na kuziteka hisia za wananchi wengi wa Tanzania kwani ilikuwa ikiwahusisha viongozi wa ngazi za juu serikalini kwa kashfa ya kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza bila kufuata kanuni.

Mawaziri hao wamepelekwa katika gereza la Keko jijini Dar es Salaam.

Aliyekuwa waziri wa fedha Bazil Mramba akatiwa hatiani katika mashitaka yote 11 yaliyokuwa yakimkabili ambapo mashitaka 10 yalikuwa ni ya matumizi mabaya ya madaraka na shitaka la 11 likiwa ni kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11. 7 sawa na takribani dola elfu tano za Marekani.

Daniel Yona aliyepata kuwa Waziri wa nishati na Madini, naye akitiwa hatiani kwa makosa matano ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara serikali.

Mshitakiwa mwingine wa tatu ambaye alikuwa katibu Mkuu wa zamani wa wizara ya fedha ya Tanzania, Aggrey Mgonja aliachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yote 11 yaliyokuwa yakimkabili.