Kicheko kwa wajasiriamali Dodoma

Image caption Kicheko kwa wajasiriamali Dodoma

Mji wa Dodoma unaonekana kuwa na sifa kadhaa katika siasa na maisha ya watanzania.

Ndio mji mkuu wa Tanzania, kijiografia ndio katikati ya nchi hiyo na vile vile, bunge la Tanzania pia liko mjini Dodoma.

Lakini mbali na sifa hizo, ipo sifa moja ambayo inaufanya mji huyo hivi sasa kuwa gumzo huku macho yote ya watanzania yameelekezwa huko.

Ndipo ambapo mikutano ya chama tawala Cha CCM inatarajiwa kuanza kufanyika kwa ajili ya kumtafuta mgombea urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

Hata hivyo, mbali na tukio hilo kubwa la kisiasa ambalo linatarajiwa kuanza kufanyika, kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo zimejitokeza katika mji huo ambao mpaka hivi sasa unaonekana kulemewa kutokana na wingi wa wajumbe na wageni mbali mbali ambao wameanza kumiminika.

Image caption Biashara imenoga

Biashara

Msemo wa jadi maarufu kama mgeni akija mwenyeji apone, unaonekana kuleta maana kamili katika kipindi hiki.

Takriban nyumba zote za kulala wageni zinaripotiwa kujaa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Aboubakar Famau ambaye kwa sasa yuko Mkoani Dodoma amezunguka katika baadhi ya nyumba za kulala wageni maarufu kama ''Guest'' na kubaini kwamba nyumba hizo zote zimejaa.

“Samahani huwezi kupata nyumba kaka,” alisema mmoja wa wahudumu wa nyumba ya kulala wageni.

“ Kutokana na vikao vya CCM vyumba vyote vimebukiwa wiki mbili kabla.

Image caption Kina mama nao wameona hii ni fursa ya kujiongezea kipato.

Maeneo ya hapa mjini huwezi kupata chumba kaka.”

Wajasiriamali

Kina mama nao wameona hii ni fursa ya kujiongezea kipato.

Pembezoni mwa barabara, nje ya jengo la CCM, kuna idadi kubwa ya kina mama ambao wanafanya biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali, lakini nyingi zikiwa na rangi ya kijani.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni mashati, magauni, kofia, bangili na hata fulana.

Image caption Idadi kubwa ya kina mama ambao wanafanya biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali, lakini nyingi zikiwa na rangi ya kijani.

Maria Mkwama ni mmoja kati ya wajasiriamali hao ambae amebobea zaidi katika kutengeza makapu ya shanga pamoja na shanga za kimaasai.

“Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa kipindi hiki, tunaweza kutengeza na mitaji yetu ikarudi,” anasema Maria huku akiendelea kupanga bidhaa zake.

Nae Stella Edwards ambaye licha ya kuuza bidhaa hizo, alionekana yeye mwenyewe akiwa mteja wa bidhaa zake kwani alikuwa amevaa koti lenye ranyi ya bendera ya Tanzania, kofia pamoja na fulana yenye rangi ya chama.

“Biashara ni nzuri, ila bado hapajachangamka sana, tunategemea kuanzia Alhamisi mpaka Jumapili,” alifafanua

Maandalizi

Wakati hayo yakijiri, uongozi wa mkoa nao unaonekana kujiweka sawa ili kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza.

Image caption Wapiga picha wako tayari kunakili matukio Dodoma

Chiko Galawa, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewaambia waandishi kwamba uongozi wake uko makini kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza ikiwemo kuwahakikishia wajumbe wote usalama.

Vile vile, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wajasiriamali wanafanya biashara kuwa makini na kutoa huduma zilizo bora hasa upande wa vyakula ili kuepusha kutokea kwa miripuko ya magonjwa.

Imeandaliwa na Aboubakar Famau, kutoka Dodoma.