Viongozi wa upinzani Uganda waachiliwa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kizza Besigye

Viongozi wawili wa upinzani nchini Uganda ambao walikuwa wamekamatwa mapema leo hatimaye wameachiliwa huru kulingana na mwanahabari wetu Patience Atuhaire aliyeko mjini Kampala.

Wawili hao Amama Mbabazi na Kizza Besigye waliwachiliwa huru huku ikidaiwa kuwa hakuna mashtaka yoyote yaliowekwa dhidi ya Besigye.

Hatahivyo haijabainika iwapo Mbabazi amewekewa mashtaka au la.

Aliyekuwa waziri mkuu Amama Mbabazi alikamatwa na polisi akiwa mjini Jinja mwendo wa saa moja kutoka jijini Kampala, akiwa njiani kuelekea katika mkutano wake wa kwanza wa hadhara na wafuasi wake mjini Mbale mashariki mwa nchi.

Siku ya Jumatano Polisi nchini Uganda walitoa taarifa kusema kuwa bwana Mbabazi hana ruhusa ya kufanya mikutano yoyote ya kisiasa japo alikuwa amewataarifu.

Haki miliki ya picha
Image caption Mbabazi

Bwana Mbabazi ananuia kutafuta uteuzi wa chama kinachotawala NRM kuwa mgombea wake rasmi wa urais katika uchaguzi huo wa mwezi Machi mwaka ujao.

Kwa upande mwingine wa nchi mwansiasa mwingine wa Upinzani Kizza Besigye alikamatwa na polisi akiwa nyumbani kwake.

Daktari Besigye , ambaye ni kanali mstaafu wa jeshi amewahi kuwania urais wa nchi hiyo mara tatu bila mafanikio.

Alikamatwa akiwa njiani kwenda kwa mkutano wake wa kwanza na wafuasi wa chama chake cha Forum For Democratic Change.