Ulaya yakubali kuipa Ugiriki mkopo zaidi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ulaya yakubali kuipa Ugiriki mkopo zaidi

Viongozi wa mataifa ya ulaya yanayotumia sarafu ya Euro wamekubaliana kwa pamoja kuipa Ugiriki mkopo mwengine ilikuinusuru uchumi wake usiporomoke kabisa.

Makubaliano hayo yanafuatia mazungumzo ya dharura baina ya mawaziri wa fedha wa ukanda wa Ulaya kwa nia ya kuiepusha Ugiriki kuishiwa na pesa na kuendelea kutumia sarafu moja ya Euro.

Rais wa baraza la ulaya Donald Tusk alitangaza kuwa makubaliano yameafikiwa baada ya mazungumzo hayo marefu yaliyochukua takriban saa kumi na saba.

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Rais wa baraza la ulaya Donald Tusk akitangaza makubaliano hayo

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa makubaliano yameafikiwa ambayo yatahitajika kudhinishwa na mabunge kadha ikiwemo bunge la Ugiriki

Bwana Tusk amesema kuwa kila kitu sasa kiko tayari kwa mabadiliko makubwa na kwa msaada wa kifedha kwa Ugiriki.

Amesema kuwa mawaziri wa fedha wa nchi za ulaya zinazotumia sarafu ya Euro watalishughulikia kama suala dharura kuisaidia Ugiriki kupata mahitaji yake ya kifedha katika kipindi cha karibuni.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuwa barabara iliyoko mbele inaweza kuwa ndefu

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuwa barabara iliyoko mbele inaweza kuwa ndefu, Lakini amesema kuwa amani itapatikana tena.

Mwandishi wa BBC barani ulaya anasema kuwa makubaliano hayo yanamaanisha kuwa Ugiriki sasa ''ni lazima imeze tembe iliyo chungu''.

Ugiriki italazimika kuimarisha utozwaji kodi,kupunguza malipo ya uzeeni na kutekeleza mabadiliko katika sera za wafanyikazi.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Viongozi wa Ulaya wakijadiliana na waziri mkuu wa Ugiriki

Aidha taifa hilo litalazimika kuwajibikia madeni iliyochukua na kuhakikisha imeweka mikakati dhabiti ya kuyalipa.

Iwapo itatekeleza mabadiliko hayo, Ugiriki itapokea Euro bilioni 95 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Haki miliki ya picha epa
Image caption Bwana Tsipras amekiri kuwa sasa ni wakati wa kufanya maamuzi magumu ya sera zake

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ana matumaini kuwa makubaliano yaliyoafikiwa yataokoa mabenki nchini humo yasiporomoke.

Aidha bwana Tsipras amekiri kuwa sasa ni wakati wa kufanya maamuzi magumu ya sera za Ugiriki.

Nchini Ugiriki kwenyewe, waziri anayehusika na na mageuzi hayo, George Katrougalos, amesema ni wazi kwamba Ulaya inayopendelea hatua za kubana matumizi imeshinda.

Amesema makubaliano hayo ya nchi zinazoitumia euro yameidhinishwa kwa lazima dhidi ya Ugiriki na kwamba itabidi nchi hiyo ikubali au ikabiliwe na kuporomoka kwa uchumi wake.