Wasifu wa makamu wa rais wa Tanzania Samia Hassan

Image caption Historia ya Samia Suluhu Hassan wa CCM

Bi Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa makamu mpya wa rais Tanzania na kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza kabisa kushikilia wadhifa huo nchini humo.

Lakini Bi Samia ni nani?

Bi Samia Suluhu alizaliwa Januari 27, 1960 visiwani Zanzibar. Alisomea shule za msingi za Chawaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) na kati ya 1966 na 1972 na kisha akasomea masomo ya upili Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976).

Alisomea kozi mbalimbali hadi akafikia kupata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani.

Kazi

Aliajiriwa kama mchapishaji katika serikali ya Zanzibar mwaka 1977 na akapanda ngazi hadi kuwa afisa wa mipango serikalini kati ya 1987 na 1988.

Alihudumu pia kama meneja wa mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Zanzibar kati ya 1985 na 1997, na pia kama meneja mkurugenzi wa Mwamvuli wa NGO 1998 hadi 1999.

Bi Samia anasema kuwa njia yake ya ufanisi haijakuwa rahisi kama inavyodhaniwa.

''Safari yangu katika siasa imekuwa njia ndefu na yenye tija.''

Kimsingi ufanisi wangu katika siasa za Tanzania umetokana na uweledi na umakini katika kila jambo ninalolifanya.''

''Sio rahisi kuwajibikia familia yako wakati huohuo ukiendelea na maisha ya siasa elimu na majukumu mengine ya kikazi," anasema Bi Samia.

Familia

Aliolewa mwaka wa 1978, kwa Bw Hafidh Ameir, ambaye wakati huo alikuwa afisa wa Kilimo .

Walijaliwa watoto wanne.

Mmoja kati ya wanawe Wanu Hafidh Ameir (1982), ni mwakilishi maalum katika bunge la Zanzibar

Image caption Bi Hassan na Dkt Magufuli wakati wa kampeni 2015

Siasa

Alijiunga na siasa mwaka wa 2000.

Wakati huo alijiunga na bunge la wawakilishi la Zanzibar kama mjumbe maalum.

Haikuchukua muda mrefu nyota yake ikaanza kung'aa na akateuliwa kuwa waziri na rais Amani Karume, akipewa wadhifa wa Waziri wa Leba, Jinsia na Watoto.

Alitumikia taifa hadi mwaka wa 2005 alipochaguliwa tena na kuteuliwa upya kama waziri, wakati huu akipewa wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji katika serikali ya visiwani.

Mwaka wa 2010 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi.

Punde tu akateuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa maswala ya muungano katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihudumu chini ya Makamu wa Rais Mohamed Gharib Bilal.

Machi mwaka 2014, aliwania na kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba nmjini Dodoma. Bi Hassan alichaguliwa kwa kura 390 sawa na asilimia 74.6 na kumshinda mpinzani wake Amina Abdalla Amour ambaye alipata kura 126 sawa na 24%.

Julai mwaka 2015, Dkt John Magufuli alimteua kuwa mgombea mwenza.

Wale wanaomjua Bi Hassan wanasema kuwa ni mchache wa maneno.