UN imetimiza lengo la kupunguza Ukimwi

Haki miliki ya picha thinkstock
Image caption UN imetimiza lengo la kupunguza Ukimwi

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon, amepongeza mafanikio ya kampeni ya kusitisha na kupunguza janga la Ukimwi.

Alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya pamoja yampango wa Umoja huo wa virsui vya HIV na ukimwi huko Addis Ababa.

Ripoti hiyo inasema mwitikio duniani dhidi ya virusi hivyo umezuia maambukizi mapya ya watu milioni 30 na takriban vifo milioni 8 tangu mwaka 2000.

Miaka kumi na mitano iliyopita, Ukimwi ulikuwa sawa na hukumu ya kifo kwa yeyote aliyekuwa nao.

Mtu yeyote aliyepatikana na maradhi hayo alijua wazi angeishia kaburini katika miaka michache tu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ban Ki Moon, amepongeza mafanikio ya kampeni za kusitisha janga la Ukimwi.

Wengi wa watoto walioambukizwa hawakufika umri wa miaka mitano.

Michel Sidibe, mkurugenzi mkuu wa shirika la umoja wa mataifa linalopambana na ukimwi, UNAIDS, amesema wengi hawakuzungumzia ugonjwa huo.

watu waliokuwa wakidhaniwa kuwa na pesa nyingi ndio waliopata fursa ya kupata dawa za kupunguza makali.

Lakini kufikia sasa, watu milioni 15 kote duniani wanapata dawa hizo kila siku na hivyo maisha yao yamerefushwa.

Urefu wa maisha nchini Zimbabwe, kwa mfano, umeongezeka kutoka miaka 44 hadi 60.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Watu milioni 15 kote duniani wanapata dawa za kupunguza makali ya ukimwi

Cuba imekuwa nchi ya kwanza duniani kuangamiza maambukizi ya ukimwi miongoni mwa watoto.

Hata hivyo, thuluthi mbili ya watoto katika mataifa mengine hawapati dawa za kupunguza makali ya ukimwi kwasababu ni kiwango kidogo tu cha madawa hayo yanayotengenezwa.

UNAIDS inasema fedha zaidi zinahitajika kuangamiza ukimwi duniani.

Shirika hilo linalenga kufanya hivyo ifikapo mwaka wa 2030.