Marekani yawaua wanajeshi wa Afghanistan

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Shambulizi la anga la Marekani lasababisha vifo vya wanajeshi 8 wa Afghanistan

Takriban askari wanane wa Afghanistan wamekufa katika shambulio la anga la Marekani kwenye kituo cha kijeshi cha ukaguzi katika jimbo la Logar kusini mwa mji mkuu Kabul, kwa mujibu wa maafisa wa Afghanistan.

Wanasema helikopta za Marekani zilishambulia kituo hicho cha ukaguzi wakati wa mchana Jumatatu.

Wanajeshi kadhaa wamejeruhiwa.

Kamanda wa jeshi katika eneo hilo ameiambia BBC kuwa kituo hicho cha ukaguzi kilikua kinapeperusha wazi bendera ya Afghanistan.

Hali ya usalama katika jimbo la Logar inayumba ambapo maeneo mengi ya vijijini vimo mikononi mwa wapiganaji wa Taliban.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanajeshi kadhaa wamejeruhiwa.

Mwandishi wa BBC David Loyn aliyeko mjini Kabul anasema kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu tukio la leo asubuhi katika wilaya ya Baraki Barak .

Mwandishi wetu anasema juhudi za uokozi zinatatizwa na makundi ya waasi wanaowashambulia kwa risasi wanajeshi wa Afghanstan.

Msemaji wa vikosi vya kimataifa nchini humo anasema wanafahamu kuhusu tukio hilo linalovihusisha vikosi vya Marekani na kwamba wanalifanyia uchunguzi.