Obama:Waandamana Nairobi

Image caption Wadai hawakufidiwa baada ya kunusurika

Saa chache tu kabla ya rais wa Marekani Barack Obama kuwasili nchini Kenya, maoni tofauti yameonekana katika mji mkuu wa Nairobi.

Kumekuwa na maandamano ya wahanga wa shambulizi la bomu la mwaka wa 1998.

Wale walionusurika katika shambulizi hilo la kwanza nchini Kenya wamekuwa wakiandamana nje ya mabaki ya jengo lililokuwa ubalozi wa Marekani.

Rais Obama anatarajiwa kuweka shada la maua kwenye mabaki ya jengo hilo.

Image caption Wanadai kuwa serikali ya Marekani iliahidi kuwalipa fidia lakini haikutekeleza ahadi yao.

Wahanga hao wanadai kuwa serikali ya Marekani iliahidi kuwalipa fidia lakini haikutekeleza ahadi yao.

Kiongozi wa kundi hilo lililokuwa likiandamana George Thigi anasema ''Nia kuu ya magaidi ni kusababisha uchungu hofu na kuua,lakini sasa iwapo serikali iliahidi kuwafidia wale waliojeruhiwa ilikupunguza uchungu wao na kisha ikakwepa majukumu yake sisi tutamlilia nani ?

''Ninaamini kuwa tukifidiwa tusihangaike magaidi hawatakuwa wametekeleza wajibu wao'' alisema Thigi.

Katika shambulizi la kwanza la kigaidi nchini Kenya,lililolenga ubalozi huo wa Marekani zaidi ya watu mia mbili walipoteza maisha yao.

Swala ambalo linahakika ya kuzua mgongano ni lile la wapenzi wa jinsia moja.

Katika mahojiano ya kipekee na rais Obama mwandishi wa habari wa BBC Jon Sopel alipomuuliza iwapo atalizungumzia ilhali anafahamu fika kuwa ni swala linalohofiwa kugawanya wenyeji wake Obama alimjibu '' hakubaliani kamwe na msimamo wa naibu wa rais wa Kenya bwana William Ruto kuwa watu hao ni ''wachafu''

Image caption Waandamana Nairobi kupinga jinsia moja

Obama hata hivyo alisema kuwa atakutana na bwana Ruto.

''Nimewahi kuwa katika hali sawa na hiyo nilipozuru Senegal''

'Licha ya kuwa miongoni mwa watu wenye mtazamo tofauti nilishikilia hoja yangu ya kuwa kila mtu anastahili kutunzwa na kuheshimiwa chini ya sheria ya usawa''alisema Obama.

Kundi la waandamanji wanaopinga sera zake za mapenzi ya jinsia moja wanamtaka Obama aheshimu tamaduni za wakenya na akome kuwashurutisha wakenya kukubali tamaduni hiyo mpya.

Vilevile, Mkamu wa rais William Ruto amemtaka asizungumzie swala hilo ''kwani inakiuka mipango ya mungu''