Mapendekezo ya amani Sudan-K yatangazwa

Wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini Haki miliki ya picha AFP

Wapatanishi wa kimataifa katika vita vya Sudan Kusini wametangaza mapendekezo yao ya makubaliano ya amani.

Wanatumai kuishawishi serikali na wapiganaji kutia saini makubaliano hayo ifikapo tarehe 17 Agosti.

Kufuatana na mapendekezo hayo Salva Kiir atabaki kuwa rais wa serikali ya mpito na kiongozi wa wapiganaji, Riek Machar, atateuliwa kuwa makamo wa rais.

Kiongozi wa wapiganaji atapata thuluthi ya viti vya baraza la mawaziri na kuwa na wingi katika serikali za mitaa, kwenye majimbo matatu yaliyoathirika zaidi na vita.

Majeshi ya pande zote mbili yatakuwa na uongozi mmoja katika mwaka-mmoja-na-nusu ujao, na kikosi kisichopendelea upande wowote kitalinda mji mkuu, Juba.

Pande zote mbili zimelalamika juu ya mpango huo, lakini zinachagizwa zaidi kimataifa kukubali muafaka huo.