Tembe ya kuavya mimba ni halali Canada

Haki miliki ya picha Science Photo Library
Image caption Tembe ya kuavya mimba ni halali Canada

Wizara ya afya ya Canada imehalalisha dawa ya kuavya mimba inayofahamika kama RU-486.

Tembe hiyo inayojumuisha dawa aiana ya ''misoprostol na mifepristone''imekuwa ikisubiri idhini hiyo tangu mwaka wa 2012.

Imekuwa ikitumika kuavya mimba Marekani tangu mwaka wa 2000.

Huko Ufaransa imekuwa ikitumika tangu mwaka wa 1988.

Viongozi wa shirikisho la kitaifa la kuavya mimba (National Abortion Federation) bi Vicki Saporta amesema kuwa hiyo ni ''habari nzuri zaidi kuwahi kutokea nchini humo''.

Hata hivyo wanaharakati wanaopinga kuhalalishwa kwa dawa hiyo ya kuavya mimba wamepinga kauli hiyo ya wizara ya Afya wakisema ni sawa na kuhalalisha ''dawa ya kuuwa binadamu''.

Tembe hiyo inatoa mimba inapomezwa na mwanamke mjamzito katika kipindi cha miezi ya kwanza tatu ya ujauzito.

Mimba za mapema ndizo zinazopigiwa upatu na wanaharakati wanaoendesha kampeini za kuhalalishwa uhuru wa kuavya mimba.

Tembe hiyo inatumika katika mataifa 60.

Nchini Uingereza tembe hiyo imekuwa ikitumika na wanawake kwa miaka 25 sasa.

Wizara ya Afya ya Canada imeithibitishia shirika la habari la BBC kuwa kutokana na kauli hiyo ya kuhalalishwa kwa tembe hiyo ya kuavya mimba kampuni inayoitengeza

Haki miliki ya picha nocredit
Image caption Tembe hiyo inatoa mimba inapomezwa na mwanamke mjamzito katika kipindi cha miezi ya kwanza tatu ya ujauzito.

Linepharma pharmaceutical sasa imepewa idhini ya kutengeza idadi kubwa ya tembe hiyo chini ya nembo ''Mifegymiso''.

Wanawake wanaotaka kuavya mimba hawatakuwa na budi ila kupimwa na daktari kabla ya kupata idhini ya kununua tembe hiyo ya ''Mifegymiso''.

''Mifegymiso'' inasemekana kuwa bora zaidi ikimezwa kabla ya kukamilika kwa siku 70 za kwanza za ujauzito.

Bi Saporta anasema kuwa tembe hiyo ya ''Mifegymiso'' itakuwa tayari kutumika ifikapo mwaka wa 2016.

Kauli yake hata hivyo inapigwa sana na bwana Jim Hughes, ambaye ndiye kiongozi wa muungano wa mashirika yanayopinga uhuru wa kuavya mimba '' Campaign Life Coalition'',

''dawa hivyo ya ''Mifegymiso''inaangamiza binadamu mbali na kumdhuru mama mjamzito,dawa hiyo sio nzuri kamwe''alisema Hughes.