Zimbabwe:Tunamtaka aliyemuua 'Cecil'

Haki miliki ya picha epicture
Image caption Zimbabwe inamtaka mwindaji aliyemuua simba maarufu Cecil arejeshwe huko iliajibu mashtaka dhidi yake

Zimbabwe inaitaka Marekani imrejeshe raia wake anayeshtumiwa kwa kuua simba ambaye alikuwa nembo ya uhifadhi wa wanyama wa porini nchini Zimbabwe ili ajibu mashtaka yanayomkabili.

Waziri wa mazingira wa Zimbabwe Bi Oppah Muchinguri amewaambia waandishi wa habari kuwa mwindaji huyo raia wa Marekani daktari Walter Palmer anastahili kufikishwa kizimbani kwa kosa alilofanya.

Daktari wa meno, Walter Palmer, anashtumiwa kwa kuua simba almaarufu 'Cecil' ambaye alikuwa ni kivutio kikubwa cha watalii nchini Zimbabwe.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Palmer anapaswa kushtakiwa kwa kosa alilofanya ;Zimbabwe

Daktari huyo wa meno na mtu mwenye uraibu wa uwindaji wa wanyama pori anasemekana kuwa alitoa hongo ya dola $50,000 iliapewe ruhusa ya kumwinda na hatimaye kumua Cecil.

Daktari Palmer anasema kuwa anajuta kwa kuua simba huyo maarufu Cecil, na kuwa alidhani ''ilikuwa mawindo halali''.

Waziri bi Muchinguri alimtaja bwana Palmer kuwa 'mwindaji haramu wa kigeni''

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu wawili waliomsaidia Palmer kuwinda cecil wameshtakiwa kwa uwindaji haramu

Hapo Jana dakta Palmer aliwaomba radhi wateja wake katika jimbo la Minnesota,ambao waliandamana kuonesha gadhabu yao kwa tukio hilo ambalo linapigwa msasa kubaini iwapo ni uwindaji haramu ama uwindaji halali.

Hatima yake itaamuliwa karibuni na ndiyo itakayotoa mwelekeo iwapo dakta Palmer atafunguliwa mashtaka au la.

Tayari wanaume wawili wanakabiliwa na mashtaka ya uwindaji haramu nchini Zimbabwe kwa kumsaidia daktari Palmer kutekeleza mauaji ya simba huyo maarufu nchini Zimbabwe.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waandamanaji nchini Marekani wanataka hatua ichukuliwe dhidi ya Palmer

Simba huyo,Cecil,alitegwa na kuuawa nje kidogo ya mbuga ya wanyama ya kitaifa ya Hwange.

Simba huyo anaaminika kuwa aliuawa Julai mosi lakini mwili wake uliokuwa ukioza ulipatikana majuzi tu.