MH370: Tony Abbot asema kitendawili karibu kitateguliwa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kipande kinachosadikiwa kuwa sehemu ya ubawa wa MH370

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amesema kuwa 'kitendawili' cha kutoweka kwa ndege ya Malaysia MH370 sasa kinakaribia kuteguliwa baada ya Malaysia kutangaza kuwa kipanda cha mabaki ya ndege hiyo kilichopatikana katika kisiwa cha Reunion cha ndege hiyo ambayo haijulikani ilipo.

Waziri mkuu Najib Razak amesema kuwa wataalam wanaochunguza mabaki hayo nchini Ufaransa wamethibitisha kwa kauli moja kwamba yametoka kwa ndege hiyo.

Hata hivyo wachunguzi hao wamejiepusha kusema kwa uhakika kwamba mabaki hayo ni ya ndege hiyo wakitaja tu kwamba inawezakana yametoka kwenye ndege hiyo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mabaki ya ndege hiyo yakisafirishwa hadi kambi ya kijeshi mjini Toulouse

Australia imesema kuwa bado ina uhakika kwamba eneo ambalo inafanyia upekuzi ni sahihi.

Ndege hiyo ya shirika la Malaysia ilikuwa ikisafiri kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing tarehe 8 Machi mwaka 2014 wakati ilipotoweka kwenye mitambo ya rada. Ilikuwa imewabeba watu 239.

Jamaa za watu waliokuwa kwenye ndege hiyo wamesema kupatikana kwa mabaki hayo 'hakuna maana yoyote''

Mabaki hayo yaliyopatikana katika kisiwa cha bahari Hindi kinachomilikiwa na Ufaransa wiki moja iliyopita- ni sehemu ya ubawa wa ndege inayojulikana kama flaperon.

Kipande hicho kilisafihwa katika maabara ya kijeshi katika mji wa Toulouse nchini Ufaransa ambako wataalam walikuwa wakifanyia uchunguzi kwa siku ya pili.