Hizi dola 1,000,000 ni za nani?

Polisi nchini Angola wanamtafuta mmiliki wa mkoba uliopatikana kwenye ndege ukiwa na dola milioni moja sawa na £650,000, ambao uliachwa kwenye ndege iliyokuwa ikisafiri hadi mjini Beijing, Uchina.

Rubani wa ndege hiyo alipata mkoba huo na kusalimisha pesa hizo kwa maafisa. Nchini Angola ni haramu kusafirisha kiasi hicho cha pesa kuvuka mipaka ya kimataifa.

Msemaji wa polisi Aristofanes dos Santos amesema kuwa uchunguzi sasa umeanzishwa kubaini asili ya pesa hizo ambazo zimetwaliwa na serikali.

Wachambuzi wanasema kuwa yeyote atakayedai kumiliki pesa hizo ataweza tu kurejesha asilimia 1.5% ya jumla ya pesa zote huku akikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha pesa kinyume cha sheria.