Mali:Hoteli zashambuliwa katika mji wa Savere

Watu waliojihami kwa bunduki wameshambulia zaidi ya hoteli mbili katika mji wa Sevare eneo la katikati mwa Mali. Walioshuhudia kisa hicho wameiambia BBC kwamba watu hao walikuwa wakiendesha pikipiki. Wakaazi sasa wamejificha katika nyumba zao na haijabainika kama kumekuwa na majeruhi.

"Tulisikia mtu akipiga mayowe kwenye kipaza sauti akiamuru kila mmoja kuingia ndani ya nyumba. Kisha tukasikia milio ya risasi" mmoja wa wakaazi amesema.

Mji wa Sevare una kituo cha jeshi la anga pamoja na wanajeshi kadhaa wa kikosi cha umoja wa mataifa cha kulinda amani.