Kimbunga chasababisha vifo vya watu 9 China

Haki miliki ya picha
Image caption Kimbunga chasababisha vifo vya watu 9 China

Utawala wa jimbo la Zhejiang lililoko Mashariki mwa China umethibitisha vifo vya watu 9 kutokana na athari za kimbunga kinachoendelea kuponda pwani yake.

Maafisa wanasema kuwa Mafuriko ,tope zito na maporomoko ya ardhi yamekumba maeneo hayo baada ya mvua kubwa ikiandamana na upepo mkali kulikumba eneo hilo.

Maelfu ya watu wamelazimishwa kuhama makwao kufuatia mvua kubwa iliyoleta hatari ya kutokea mafuriko.

Katika maeneo yaliyoko chini karibu na bahari kumeripotiwa mvua kubwa takriban centimita 50 katika kipindi cha saa ishrini na nne zilizopita.

Haki miliki ya picha
Image caption Uharibifu uliosababishwa na kimbunga

Kiwango hicho cha mvua ni cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa zaidi ya karne moja iliyopita.

Kimbunga hicho kikali kimesababisha hali ya wasiwasi katika maeneo kadhaa Kusini mashariki mwa Uchina ambapo watu wengi wameachwa bila umeme na maji.

Katika Mkoa wa Fuji upepo mkali ulioandamana na mvua umeacha barabara kadha zimefungika na mafuriko kila mahali.

Safari za ndege na gari moshi zimesitishwa na kuwaacha mamia ya watu bila njia ya usafiri.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Karibu watu 160,000 wamehamishwa kutoka makaazi yao.

Karibu watu 160,000 wamehamishwa kutoka makaazi yao.

Awali kimbunga hicho kilisababisha maafa sawa na hayo katika taifa jirani la Taiwan, ambapo mamilioni ya watu hawana umeme baada ya kimbuga hicho kupiga kisiwa chote Jumamosi asubuhi.

Zaidi ya miti 2,000 iling'olewa katika kisiwa cha Taipei kutokana na kimbunga kikubwa zaidi kuwahi kutokea eneo hilo.