Miaka 130 jela kumuambukiza mtoto Ukimwi

Image caption Miaka 130 jela kumuambukiza mtoto Ukimwi

Mahakama moja nchini Kenya imemhukumu mwanaume mmoja kifungo cha miaka 130 jela kwa kumbaka na kumuambukiza mtoto mwenye umri wa miaka 9 ukimwi.

Katika kikao hicho Mahakama kuu ya Kenya mjini Kisumu imempata na hatia bwana John Okewo mwenye umri wa miaka 25 na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 9 ambaye jina lake limebanwa.

Hakimu mwandamizi Aswani Opande alimpata na hatia bwana Okewo kwa kumabaka mtoto huyo na akamhukumu kifungo cha miaka 100 jela.

Katika shtaka la pili hakimu huyo mkuu wa eneo la Tamu lililoko Muhoroni alimhukumu mstakiwa kifungo cha miaka mingine 30 kwa kumuambukiza msichana huyo mwenye umri wa miaka 9 ugonjwa wa Ukimwi.

Hakimu alimpata na hatia bwana Okewo kutokana na kukiri makosa yake mwenyewe.

Upande wa mashtaka unasema kuwa bwana Okewo alimpa mtoto huyo pipi na biskuti mnamo tarehe 27 mwezi Machi kabla ya kumdanganya hadi akaingia chumbani mwake.

Yamkini Okewo aliwaambia wachunguzi kuwa alimdhulumu mtoto huyo mara kadha.

Image caption Mtoto huyo alimtambua mshtakiwa kuwa mtu aliyemnunulia pipi biskuti na ''kumlalia''

Mtoto huyo alimtambua mshtakiwa kuwa mtu aliyemnunulia pipi na ''kumlalia''

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 9 anaendelea na matibabu maalum ya wanawake baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo.

Alipopewa fursa ajitetee, mshtakiwa aliomba asamehewe kwani ni ''shetani aliyemdanganya'' kutenda maovu hayo.

Hata hivyo Hakimu akakataa kabisa kumuonea huruma na akamhukumu kifungo cha miaka 130 jela ili iwe funzo kwake na kwa wengine wenye mawazo potofu kama yake.

Alipewa siku 14 kukata rufaa.