Al Qaeda:Mwana wa Bin Laden atoa ujumbe

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Osama Bin Laden

Kundi la kigaidi la A Qaeda limetoa ujumbe wa sauti ambao unadai kwamba umetoka kwa Hamza Bin Laden ,mwana wa Osama Bin Laden.

Ujumbe huo unaaminika kuwa wa kwanza wa propaganda za Al Qaeda kumshirikisha Hamza Bin Laden kama mwanachama wa kundi hilo.

Katika ujumbe huo uliosambazwa na Al Qaeda katika mtandao wa twitter,Hamza Bin Laden anaagiza mashambulizi dhidi ya Marekani na washirika wake.

Osama bin Laden aliuawa na vikosi maalum vya Marekani mnamo mwaka 2011 katika uvamizi nyumbani kwake huko Abbotabad,Pakistan.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanajeshi maalum wa Marekani wakati walipovamia makaazi ya Osama Bin Laden huko Pakistan

Kundi hilo limekuwa likiongozwa na naibu wake Ayman al-Zawahiri.Uwepo wa Hamza Bin Laden haujulikani,anadaiwa kuwa mwenye umri wa miaka ya 20.

Wakati wa uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan mwaka 2001,shirika la habari la Al-Jazeera lilionyesha picha yake miongoni mwa wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan.

Ujumbe wake wa sauti uliotolewa na Al Qaeda unawataka wafuasi wake mjini Kabul,Baghdad na Gaza kuanzisha jihad ama vita vitakatifu mjini Washington,London,Paris na Tel Aviv.