Watu 19 wauawa kwa Bomu Bangkok

Image caption Eneo lililotokea shambulio la Bomu ni maarufu kwa kuwa hupendwa sana na watalii

Polisi nchini Thailand wamesema takriban watu 19 wameuawa kwa shambulizi la bomu katika Hekalu maarufu la jamii ya Hindu mjini Bangkok.

Zaidi ya watu 120 wamejeruhiwa.Ripoti zinasema bomu hilo lilibebwa kwenye pikipiki.

Mlipuko huo uliotokea karibu na Hekalu la Erawan ulisababisha taharuki katika eneo hilo maarufu kwa utalii.

Waziri wa ulinzi Prawit Wongsuwan amesema walipuaji hao waliwalenga wageni ili kuharibu utalii na uchumi. Taarifa zinasema mabomu mengine katika eneo la utalii yaliteguliwa.

Hakuna kundi lolote lililokiri kufanya mashambulizi hayo mjini Bangkok.

Tangu miaka ya 1960 mashambulizi yamekuwa yakitekelezwa kusini mwa Thailand, ambako kumekuwa na mfululizo wa mashambulizi ya mabomu ya kutegwa kwenye gari kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.