Rais wa Gabon ametoa urithi wake kwa umma

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rais wa Gabon ametoa urithi wake kwa vijana wa Gabon

Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba ameahidi kutoa urithi wake wote kwa vijana nchini humo.

Ali anasema kuwa mali yote aliyopokea kama urithi kutoka kwa babake mzazi aliyekuwa rais wa Gabon kwa kipindi kirefu,Omar Bongo itakwenda kwa vijana wa Gabon.

Shirika la habari la AFP limesema kuwa rais Bongo ameahidi kuuza mijengo miwili iliyoko Ufaransa aliyopewa na babake kwa thamani ya Franka moja kama ishara ya kujitolea kuimarisha hali ya kiuchumi ya vijana wa taifa.

Jumba moja la kifahari lililoko katika mji mkuu wa taifa hilo litabadilishwa na kuwa chuo kikuu cha Umma.

Majumba mengine mawili yako mjini Paris Ufaransa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Majumba mawili yako mjini Paris Ufaransa na lingine liko Gabon.

Kauli hiyo ya rais Bongo inawadia wakati ambao majaji nchini Ufaransa wamekuwa wakifuatilia na kuchunguza chanzo cha mamilioni ya fedha zilizotumika kununua na kujenga majumba ya kifahari nchini humo.

Wapinzani na wanaharakati wa kupambana na ufisadi wanasema kuwa huenda rais Ali Bongo Ondimbaameona kibano kinachokuja akaamua kuirejeshea taifa maili yake.

Shirika la kupigana na ufisadi, Transparency International liliwasilisha kesi mahakamani likitaka majaji hao waamuru kuwa mali ya umma ilitumika kujistawisha wakati wa utawala wa babake marehemu rais Omar Bongo.

Babake marehemu rais Omar Bongo alitawala nchi hiyo kwa miaka 40.