Uhaba wa kondomu Zanzibar ?

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Upungufu wa kondomu Zanzibar ?

Kondomu imeonekana kuwa ni bidhaa adimu mjini Unguja visiwani Zanzibar.

Hii inatokana na kuwa matumizi yake yanaonekana kuwa mwiko.

Tofauti na miji mingine mikubwa ya bara, nchini Tanzania kama mji mkuu wa Dar es Salaam,ambako karibu kila kioski mtaani kinauza bidhaa hiyo, visiwani Zanzibar ambapo karibu zaidi ya asilimia 90 ya wakazi ni waumini wa dini ya Kiislamu, wauzaji wa vioski vidogo vidogo mtaani wanaona kuuza kondomu ni sawa na kupigia chepue vitendo haramu vya ngono na zina.

Mwandishi wa BBC Sammy Awami, alifuatilia swala hili alipokuwa Zanzibar siku chache zilizopita

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kila kitu kinachowezesha zinaa na kuchangia faida itokanayo na zina ni haramu kulingana na dini ya Kiislamu '' alisema muuza duka kisiwani Zanzibar

Zanzibar ni kisiwa kilichoneemeka kwa kuwa na vivutio kedekede na hivyo kutembelewa na maelfu ya watalii kila mwaka.

Lakini yapo pia matamasha kama Sauti za Busara, ama hili la filamu ZIFF lililomalizika hivi karibuni, ambayo hukusanya maelfu ya mashabiki kwa wakati mmoja.

Katika mikusanyiko hii, bila shaka vitendo vya kujamiana vinatarajiwa kushamiri.

Hata hivyo BBC iling’amua kwamba upatikanaji wa kondomu visiwani humo si wa rahisi.

Haki miliki ya picha bbc wasawat lokharang
Image caption Uhaba huo unatokana na msimamo wa kidini

Katika kisiwa kilicho na idadi ya watu wapatao milioni 2 ,takriban zaidi ya asilimia 90 wakiwa ni waamini wa dini ya Kiislamu.

Wauzaji wa maduka na wazanzibari wenyewe walimwambia mwandishi wa BBC kwamba sababu kubwa ya uhaba huo wa kondomu ni dini.

''Dini yetu inakataza tendo la zina'' alisema muuzaji mmoja wa duka la rejareja.

'kila kitu kinachowezesha zinaa na kuchangia faida itokanayo na zina ni haramu '' aliongezea kusema.

Image caption Kisiwa cha Zanzibar ni kivutio kikubwa cha watalii

''Hivyo, uuzaji wa kondomu unachukuliwa kama ni kuwatia watu moyo wafanye vitendo hivyo vinavyokufuru mafundisho ya dini.''

Hata hivyo, wakati pakiwa na njia panda kati ya mafundisho ya dini na hali halisi ya hatari ya kuambukizwa magonjwa kama ukimwi,takwimu za umoja wa mataifa zilizopo zinaonesha tangu mwaka 2002 ushamiri wa maambukizi ya ukimwi na virusi vyake umesalia kuwa chini ya asilimia moja tu visiwani humo.