Wakenya wafuzu kwa fainali ya mita 5000

Image caption Wanariadha Beijing

Mashindano ya riadha ya duniani yanaendelea leo mjini Beijing Uchina.

Katika mbio za mchujo za mita 5,000 kwa kina dada wanariadha wote wa Kenya wamefuzu kwa fainali.

Wanariadha hao ni pamoja na Viola Kibiwot, Mercy Cherono, Irene Cheptai na Janet Kisa.

Hata hivyo wanariadha hao wa Kenya wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanariadha wa Ethiopia, ambao wote waliandikisha muda wa kasi zaidi kati mbio hizo zilizoandaliwa mapema hii leo.

Almaz Ayana aliandikisha muda wa dakika 15:09.40 naye Senbere Teferi alizitimuka mbio hizo kwa muda wa dakika Mshindi wa medali ya fedha katika mbio za mita 10,000, Genzebe Dibaba pia alifuzu kwa fainali hizo na kuimarisha matumaini yake ya kunyakuwa medali mbili katika mashindano ya mwaka huu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Genzebe Dibaba wa Ethiopia

Mwanariadha mwingine kutoka bara la africa Olivia Mugove kutoka Zimbabwe aliyaaga mashindano hayo baada ya kumaliza katika nafasi ya 12, katika mchujo wa kwanza.

Jumla ya wanariadha 15, watapambana katika fainali itakayoandaliwa siku ya Jumapili.

Msimamo wa medali

Kufikia sasa Kenya bado ingali kileleni mwa msimamo wa medali ikiwa na jumla ya medali kumi na moja.

Sita za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba.

Uingereza ni ya pili na medali tatu za dhahabu, ikifuatwa na Jamaica ikiwa na medali mbili za dhahabu na moja ya fedha.

Cuba ni ya nne nayo Marekani ikikamilisha orodha ya nchi tano bora.

Ethiopia inashikilia nafasi ya saba ikiwa na medali moja ya dhahabu na mbili za fedha.

Eritrea inashikilia nafasi ya kumi na medali moja ya dhahabu sawa na Afrika Kusini.

Mataifa mengine ya Afrika yaliyonyakuwa medali katika mashindano ya mwaka huu ni Misri ambayo ina medali moja ya Fedha na Uganda ambayo imejinyakulia medali moja ya shaba.