Maafisa wa Ruihai wakamatwa Uchina

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Magari yaliyoteketea Tianjin

Maafisa nchini serikali ya Uchina, wanaendeleza uchunguzi kuwatambua waliohusika katika milipuko mikubwa ya kemikali yaliyoutikisa mji wa bandari wa Tianjin mapema mwezi huu.

Watu 23 wametajwa kuhusika na hali iliyosabaisha kutokea kwa milipuko hiyo wakiwemo watu 12 wanaozuliwa na polisi.

Watu 139 waliuawa wakati ghala moja lilipoteketea moto na kulipuka na kusababisha moto mkubwa angani na kuliharibu eneo kubwa la mji huo waTianjin.

Wakurugenzi kadhaa wa kampuni ya Ruihai Logistics, iliyokuwa ikiendesha shughuli zake katika ghala hilo lililolipuka wamekamatwa na polisi.

Miongoni mwao ni mwenyekiti wa kampuni hiyo, naibu mwenyekiti na manaibu wakurugenzi wakuu watatu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Uharibifu uliotokea Tianjin baada ya mlipuko

Wengine saba ambao bado hawajatajwa pia wanazuliwa.

Wamiliki kampuni hiyo wanadhaniwa kutumia ushawishi wao kibinafsi kujipatia vibali vilivyowaruhusu kuhifadhi kemikali hatari karibu na makaazi ya watu.

Shirika la kitaifa la habari la Uchina, limearifu mapema kwamba kampuni ya Ruihai, ilihudumu kwa zaidi ya mwaka mmoja pasi na kuwa na vibali vinavyohitajika.

Maafisa 11 wa serikali pia wanashukiwa kwa uhalifu, uliosababisha milipuko hiyo kuanzia uzembe kwa kutofanya ukaguzi wa kiusalama hadi utumiaji wa mamlaka kwa kutoa vibali haramu vya kuendesha biashara.