Viongozi wa Ulaya kujadili Uhamiaji

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mawaziri wa Mambo ya nje wa Ulaya

Waziri wa mambo ya je wa Ujerumani, ameonya kuwa huenda raia wa nchi hiyo wakaghadhabishwa ikiwa idadi ndogo ya nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya, watashurutishwa kugharamia mzozo wa uhamiaji.

Frank-Walter Steinmeier aliyasema hayo mjini Viena kabla ya mkutano utakaohudhuriwa na wakuu wa serikali za Ujerumani, Austria na mataifa mengine sita yaliyoko Magharibi mwa visiwa vya Balkan.

Ujerumani inajiandaa kupokea maombi zaidi la laki nane ya uhamiaji mwaka huu, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuliko taifa lolote katika Muungano wa Ulaya.

Awali, waziri wa mambo ya nje wa Austria, alionya kwamba sehemu kuu ya sera ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya inashindwa kufanya kazi.

Sebastian Kurtz, alikuwa akizungumza na BBC kufuatia kuwadia kwa kikao hii leo kinachonuia kuratibu jitihada za kukabiliana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaoelekea Ulaya kupitia Magharibi mwa visiwa vya Balkan.

Kwa mujibu wa sheria ya Umoja wa Ulaya, waomba hifadhi ni lazima wawasilishe ombi katika nchi ya kwanza ya Ulaya wanayowasili, lakini Kurz anasema nchi maskini zaidi kama Ugiriki zinajitahidi kuwaruhusu wakimbizi wasafiri hadi katika nchi tajiri.