Muadhini mmoja matatani Misri Je kunani?

Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Muadhin akiwaalika waumini kwa sala za alfajiri

Muadhini mmoja nchini Misri, anatarajiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu, baada ya kutuhumiwa kubadili maneno yanayotumiwa kuwaalika waumini wa Kiislamu wa sala za Alfajiri.

Wizara inayohusika na masuala ya kidini nchini humo, imesema kuwa itamchukulia hatua za kisheria, Mahmoud al-Moghazi, mhubiri mmoja mjini Kafr al-Dawar iliyoko katika eneo la Nile Delta.

Muhubiri huyo anatuhumiwa kuwa badala ya kusema '' Kuomba ni bora kuliko kulala'' maneno ambayo yametumiwa tangu jadi kuwaalika waumini kwa sala za alfajiri, alisema '' Kuomba ni bora badala ya kutumia muda kwa mtandao wa kijamii wa Facebook''.

Waumini katika msikiti wa Sayed Ghazi wamewalisha malalamiko rasmi kwa serikali dhidi yake.

Kamati inayosimamia msikiti huo tayari imemsimamisha kazi huku uchunguzi ukiendelea.

Waumini wasusia sala

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Muumini akisali msikitini

Katika mahojiano kwenye runinga moja nchini humo, muumini mmoja alimshutumu muhubiri huyo kwa kuwa mzembe na mzushi.

Muumini huyo amesema kwa sababu ya kutowajibika kwa al-Moghazi, wameacha kusali katika msikiti huo.

Lakini al-Moghazi alimshutumu muumini huyo kwa kutohudhuria sala katika msikiti huo wa Sayed Ghazi na kuwa ni mfuasi wa kundi lililopigwa marufuku la Muslim Brotherhood.

Aidha Muadhini huyo ametishia kuanza mgomo wa kususia chakula kufuatia uamuzi huo wa kumsimamisha kazi na kutoa wito kwa rais wa nchi hiyo Abdul Fattah al-Sisi kuingilia kati.

Anasema hajawahi kutumia mtandao wa kijamii wa facebook hata siku moja.