Wanariadha wa Kenya warejea nyumbani

Image caption Julius Yego akikaribishwa kwa kupewa maziwa katika uwanja wa JKIA

Mbwembwe zinaendelea katika jumba la mikutano ya Kimataifa la KICC, ambako wanariadha wa Kenya wamepokewa na kuandaliwa dhifa ya chakula cha mchana na shirikisho la mchezo wa riadha nchini Kenya AK.

Kikosi hicho kilichowasili leo asubuhi kutoka Beijing ambako kiliibuka mshindi wa mashindano ya riadha ya dunia, kililakiwa na maelfu ya wakenya na wakuu wengine wa serikali wakiongozwa na makamu wa rais William Ruto.

Akihutubia dhifa iliyoandaliwa na serikali, Ruto aliwapongeza mashujaa hao walioiweka Kenya katika nafasi ya duniani katika mashindani hayo ya riadha yaliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Beijing China.

Image caption Makamu wa rais akielekea kuwakaribisha wanariadha wa Kenya katika uwanja wa JKIA

Kenya imepata dhahabu saba, miongoni mwao urushaji mkuki na mita mia nne kuruka vizuizi, mashindano ambayo ni mara ya kwanza kwa Kenya kushinda medali katika mashindano ya Kimataifa.

Image caption Wacheza danse waliowatumbukiza wanariadha wa Kenya

Dhahabu zingine zilinyakuliwa katika mbio za mita elfu kumi na kina dada, kwa upande wa wanaume ni mbio za mita mia nane , mita elfu tatu kuruka maji na viunzi na mita elfu moja mia tano.

Kenya pia ilinyakuwa medali sita ya fedha na tatu za shaba na kuweka rekodi hiyo ya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwahi kuwa mshindi wa mashindano hayo ya riadha ya dunia.

Image caption Makamu wa rais William Ruto akiwa na mshindi wa mbio za mita 400 kuruka viunzi