Guterres aomba wakimbizi waruhusiwe Ulaya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wakimbizi kutoka Syria

Kamishna wa tume ya Umoja wa Mataifa, anayehusika na masuala ya wakimbizi, Antonio Guterres, ameyaomba mataifa ya Ulaya kuwakubali wakimbizi laki mbili wanaokimbia mapigano nchini Syria, Iraq na Afghanistan.

Bwana Guterres amesema kuwa jibu lao huenda likaathiri mustakabali wa muungano wa Ulaya.

Kamishna Guterres amewasihi viongozi wa Ulaya kutafuta namna ya kuwaruhusu wakimbizi halali kuingia Ulaya kwa urahisi.

Kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa, ameonya kuwa nchi za Ulaya haziwezi kuendelea kushughulikia suala hili la wakimbizi kila moja kwa njia yake.

Amesema kuwa bara hilo likikosa kushikana kwa pamoja kuhusu suala hili watakaonufaika ni walanguzi wa binadamu na mawakala wa wahamiaji.

Haki miliki ya picha
Image caption Antonio Guteres

Awali wajumbe kutoka tume ya Ulaya, walianza ziara katika kisiwa cha Kos, nchini Ugiriki, ambako maelfu ya wakimbizi wamekuwa wakiwasili kila siku.

Wengi wa wakimbizi hao, wamelalamika kuwa inawachukua muda mrefu, kabla ya kupata stakabadhi wanazohitaji kuondoka kisiwani humo.

Serikali ya Ugiriki imeahidi kuharakisha shughuli hiyo, lakini kamishna wa Ugiriki, anayehusika na masuala ya uhamiaji amesema kuwa ni lazima mataifa yote ya Ulaya, yashirikiane kutafuta suluhisho la kudumu.

Ziara hii ya tume ya Ulaya, ndio ya punde zaidi katika msururu wa juhudi za kutafutia ufumbuzi janga la uhamiaji barani Ulaya.