Siku 100, Rais Buhari amefanikiwa?

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari

Mwisho wa juma hili, siku ya Jumamosi, rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, anatimiza siku mia moja akiwa Rais wa nchi hiyo.

Rais Buhari alimshinda Goodluck Jonathan katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Machi baada ya kuahidi kukabiliana na makundi ya ugaidi na kutokomeza kiwango kikubwa cha ufisadi.

Lakini yeye pia anakabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Muhammadu Buhari ameingia madarakani akiogelea katika wimbi la matumaini kwamba ataleta mabadiliko.

Haraka sana baada ya kuingia madarakani, aliazimia kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram, huku akibadilisha uongozi wa jeshi.

Bado ni mapema kujua iwapo kutakuwa na hali ya amani katika siku zijazo.

Haki miliki ya picha Nigerian Army
Image caption Kundi la wanamgambo, Boko Haram bado ni changamoto nchini Nigeria

Lakini kinachotia wasiwasi ni kwamba, kumekuwa na mashambulizi ya mara kwa mara na kwa Buhari kujipa muda wa miezi mitatu kupambana na Boko Haram ni kutojua ukubwa wa mgogoro huo.

Rais Buhari pia bado hajateua baraza la mawaziri, ingawa ameahidi kufanya hivyo mwezi huu.

Pia kuna wasi wasi kwamba, bila waziri wa fedha, hakuna sera ya uchumi iliyo wazi hasa katika kipindi hiki kigumu kwa taifa hilo.

Kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, serikali inapambana kuweka mahesabu yake sawa ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara kwa wafanyakazi wake.

Kuhusu uteuzi wa baraza la mawaziri, baadhi ya wachambuzi wanasema haikuwa rahisi kupata viongozi waliotimiza vigezo vya uadilifu wakati ambapo rais Buhari ana dhamira ya kupambana na rushwa.

Shirika la taifa la mafuta imekuwa ni mwanzo mzuri, baada ya kuutimua uongozi wote na kumweka mwanasheria aliyesoma Chuo Kikuu cha Havard huku akiwa na uzoefu wa sekta binafsi kuliongozi shirika hilo linaloongoza kwa rushwa.

Kumekuwa na dalili za kufanikiwa katika shirika hilo ambalo kwa muda mrefu linaonekana kutelekezwa.

Rais Buhari, kamwe hataacha hali kama ilivyo, na hii ndio fursa pekee ya kutatua baadhi ya matatizo ambao yameikwaza nchi hiyo kufikia malengo yake ya kimaendeleo.

Tusichokijua mpaka sasa, ni je, ana tiba sahihi ya matatizo ya nchi yake?