Mwelekezi wa Taylor Swift atetea video

Video ya Wildest Dreams Haki miliki ya picha Universal
Image caption Video ya Wildest Dreams iliyoandaliwa Botswana na Afrika Kusini

Mwelekezi wa video mpya ya Taylor Swift iliyoshutumiwa kwa kuonyesha picha mbaya ya Afrika amejitokeza na kuitetea vikali.

Video hiyo ya wimbo Wildest Dreams imedaiwa kuendeleza dhana potovu ya maisha bora iliyokuwa na wakoloni barani Afrika.

Lakini mwelekezi Joseph Kahn amesema "video hiyo haihusu ukoloni bali ni simulizi ya kisa cha mapenzi katika kundi la waandalizi filamu Afrika, 1950".

Swift hajazungumzia utata uliogubika video hiyo.

Kupitia taarifa, Kahn amekanusha madai kwamba video hiyo imeshirikisha Wazungu pekee.

“Ukweli ni kwamba sio tu kuwa kuna watu wa asili nyingine kwenye video hiyo, bali pia wabunifu waliofanyia kazi video hiyo ni wa asili nyingine.”

Ameeleza kuwa yeye ni wa asili ya Asia na Amerika, naye produsa wa video hiyo Jill Hardin na mhariri Chancler Haynes ni Waafrika Waamerika.

“Tuliamua kwa pamoja kwamba haingekuwa sahihi kihistoria kujaza waigizaji weusi kwenye video hiyo kwani tungeshutumiwa na kudaiwa kujaribu kuandika upya historia.

“Video hii inaonyesha mambo ya zamani kupitia watu wanaoishi kwa sasa na tunajivunia kazi yetu.”

"Kuna Waafrika weusi kwenye video hiyo, lakini sikuangazia sana watu wengine kwani muda mwingi unachukuliwa na Taylor na Scott (Eastwood).''

Video hiyo imetazamwa mara milioni 19 tangu ipakiwe mtandaoni Jumatatu.