Rais Buhari atangaza utajiri wake

Rais Muhammadu Buhari
Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akihutubu awali

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametangaza kuwa ana $150,000 (£100,000) kwenye akaunti zake za benki, katika hatua inayolenga kuendeleza uwazi na kupiga vita ufisadi serikalini.

Kiasi hicho kinaonyesha kuwa amekuwa akiishi “maisha ya kujinyima”, msemaji wake Garba Shehu amesema.

Bw Buhari anamiliki makao matano na nyumba mbili za matope, pamoja na mashamba kadha, akaongeza.

Kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi alichaguliwa kuwa rais mwezi Machi ahadi zake kuu zikiwa kukabiliana na ufisadi na ukosefu wa usalama.

Ufisadi ni tatizo sugu katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika na mwezi uliopita, Bw Buhari alisema $150bn (£100bn) zimeporwa kutoka kwa hazina ya serikali.

Bw Shehu alisema kupitia taarifa kuwa Bw Buhari ana shamba la matunda na renchi yenye ng’ombe 270, kondoo 25, farasi watano na ndege wengi.

Pia anamiliki hisa katika kampuni tatu - Berger Paints, Union Bank na Skye Bank, taarifa hiyo iliongeza.

Hata hivyo, makamu wa rais wa Nigeria Yemi Osinbajo ni tajiri kumshinda mdosi wake.

Taarifa hiyo ilisema Bw Osinbajo ana $900,000 (£600,000) kwenye akaunti zake za benki.

Kwenye fomu ya kutangaza utajiri wake, Bw Osinbajo pia alifichua anamiliki nyumba nne, moja ikiwa ya vyumba viwili vya kulala ambayo analipia mkopo mjini Bedford, Uingereza.

Taarifa hiyo haikusema thamani halisi ya mali yote ya rais na makamu wake, ikieleza kuwa stakabadhi zilizokabidhiwa Afisi ya Maadili zitafanywa wazi kwa umma karibuni baada ya ukaguzi wake kukamilika.