Askofu Tutu hatimaye arejea nyumbani

Haki miliki ya picha BENNY GOOL
Image caption Askofu Desmond Tutu akiwa hospitalini

Askofu mustaafu kutoka Afrika Kusini, Desmond Tutu, ameachiliwa kurejea nyumbani kutoka hospitalini, ambako amekuwa akipokea matibabu kwa zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Kwa mujibu wa wakfu wake, Tutu alikuwa akiuguzu maambukizi yaliyokuwa yamemkumba kwa mara kadhaa.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya nobel mwenye umri wa miaka 83, amekuwa na matatizo ya kiafya katika miezi ya hivi karibuni.

Hivi majuzi alilazwa hospitalini kutokana na maambukizi yaliyosababishwa na saratani ya tezi dume aliyokuwa akiugua.

Askofu tutu alistaafu rasmi mwaka wa 2011, lakini bado angali anasafiri kwa shughuli mbali mbali.

Taarifa iliyotolewa na wakfu wake ilisema kuwa Askofu huyo mstaafu amewashukuru wafanyakazi wa hospitali ya Cape Town kwa kumhudumia vyema.

Aidha alitoa shukrani kwa raia wa nchi hiyo kwa kumkumbuka kwa maombi yao na risala za heri njema.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Askofu Desmond Tutu

Tutu alilazwa hospitalini tarehe 20 Agosti mwaka huu wiki mbili tu baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka hospitalini.

Askofu huyo mweusi wa kwanza wa Jimbo la Cape Town alikuwa mstari wa mbele katika harakati za kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.