Wahamiaji zaidi wapokelewa Ujerumani

Wakimbizi waliowasili stesheni ya reli ya Munich, Ujerumani Haki miliki ya picha Getty

Maelfu ya wahamiaji zaidi wanaelekea Austria na Ujerumani kwa siku ya pili, baada ya kunasa kwa siku kadha nchini Hungary.

Mamia wanasafirishwa kutoka mpaka wa Austria na Hungary na wengine zaidi wamepanda treni kutoka mji mkuu wa Hungary, Budapest.

Iliarifiwa kuwa watu kama 10,000 waliingia Austria Jumamosi - tena wengi wao walielekea Ujerumani.

Katika mji wa Nickelsdorf, kwenye mpaka wa Austria, wakimbizi walipewa msaada na watu waliojitolea kama Arnold Digruber.

Anasema kinachomchoma ni mashaka yanayowakuta watoto wadogo:

"Mimi nina mvulana mdogo piya.

Hili swala linanichoma moyoni.

Samahani, lakini ukiona mashaka haya yanayowakuta, hasa familia zenye watoto wadogo.

Inasikitisha."

Makundi ya watu yalifika maeneo ya mapokezi katika miji mingi ya Ujerumani kuwashangilia wahamiaji hao.

Serikali ya mseto ya Ujerumani inakutana Jumapili kujadili mipango ya hatua ambazo Ujerumani na Umoja wa Ulaya nzima inafaa kuchukua, kushughulikia msukosuko unaotokana na wahamiaji wengi kuwasili katika bara la Ulaya.