Japan yaadhiriwa na mafuriko makubwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mafuriko nchini Japan

Mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi nchini Japan vimewalazimisha zaidi ya watu elfu 90 kuzihama nyumba zao.

Picha zilizochukuliwa kutoka maeneo yaliyoathiriwa kutoka miji ya Joso na Tokyo, zinaonyesha nyumba zilizoharibiwa na mafuriko hayo.

Wazee walionekana wakipanda kwenye paa za nyumba kabla ya helikopta za kikosi cha uokozi kuwanusuru.

Nyumba zote na magari vimesombwa na maji ya mto ujulikanao kama Kinugawa baada kingo zake kupasuka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu.

Takriban watu 12 wamejeruhiwa huku wengine wakiwa hawajulikani waliko.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Nyumba zilizofunikwa na maji

Kumekuwa na hofu kwamba huenda maji ya mafuriko hayo yakasomba sumu za kemikali ndani ya bahari kwenye mtambo wa nishati ya nuklia wa Fukushima.