Wazazi watundu matatani Afrika Kusini

Image caption Watoto wa shule

Afrika Kusini imeanza kutekeleza sheria mpya, ambayo itaidhinisha majina ya wazazi ambao hawalipi malezi ya watoto kujumuishwa kwenye orodha ya watu wasiolipa madeni.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, watu hao wasiolipa hawatapewa mikopo na taasisi yoyote ya kifedha.

Lakini wakosoaji wa sheria hiyo wanasema kuwa itafanya hali ya maisha kuwa ngumu zaidi hasa kwa watu wa mapato ya chini.

Serikali ya nchi hiyo imesema sheria hiyo itawashurutisha wale ambao hawapi watoto wao msaada kufanya hivyo.

Baada ya shutuma nyingi, kipengee hicho kiliondolewa lakini kikarejeshwa tena na tayari rais Jacob Zuma ameisaini kuwa sheria.

Miongoni mwa wale wanaopinga sheria hiyo hiyo ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Party kinachoongozwa na Julius Malema, ambaye wafuasi wake wengi ni watu wenye mapato ya chini.

Idadi kubwa ya watu nchini Afrika Kusini, hasa watu masikini hutegemea mikopo kuendeleza maisha yao.