Hungary yaaibisha Ulaya kuhusu wakimbizi

Wahamiaji watembea kwa miguu kuondoka Hungary Haki miliki ya picha AP

Kiongozi wa Austria amesema namna Hungary inavowatendea wakimbizi na wahamiaji inamkumbusha zama za ukatili katika historia ya Ulaya.

Werner Faymann alifananisha sera za rais wa Hungary, Viktor Orban, na zile zilizotumiwa na Ma-Nazi waliowafukuza Wayahudi wakati wa mauaji makubwa ya Wayahudi katika Vita vya Pili vya Dunia.

Werner Faymann piya alitoa wito kuwekwe vikwazo dhidi ya nchi zinazokataa kupokea viwango vya wakimbizi vilivyopendekezwa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Hungary inasema kutoka Jumaane, itawachukulia watu wote wanaowasili kinyume cha sheria kuwa ni wahalifu na itawakamata.

Piya imesema Umoja wa Ulaya unafaa kuzipa nchi jirani na Syria euro bilioni tatu ili kuzuwia watu kuhama kwa wingi kwenda Ulaya.

Maelfu ya wahamiaji wamekuwa wakisafiri kwa kupitia Hungary kuelekea Ulaya Kaskazini.

Shirika la uhamiaji la kimataifa, IOM, limesema wakimbizi zaidi ya 430,000 wamevuka Mediterranean tangu mwaka huu kuanza.