Ujerumani,Czech,Austria zahofia mipaka

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maelfu ya Wakimbizi wamekuwa wakiingia kwa wingi nchi za ulaya kinyume cha utaratibu

Ujerumani,Austria na jamuhuri ya Czech zimeimarisha ulinzi katika mipaka yake baada ya wakimbizi kuingia mjini Munich na maeneo mengine.

Tamko la mamlaka ya Reli ya Austria imesema safari za treni kutoka na kuingia nchini Ujerumani zimesitishwa mpaka siku ya jumatatu asubuhi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere,amesema hatua iliyochukuliwa ni ya muda mfupi tu.

Czech ambayo inatoa njia mbadala ya kuelekea Ujerumani imesema itaimarisha udhibiti katika mpaka wake na Austria.

Waziri wa mambo ya ndani,wa nchi hiyo,Milan Chovanec,amesema hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa kwa kutegemea na idadi ya wakimbizi wanaoelekea Jamuhuri ya Czech.

Waziri mkuu wa Hungary,Viktor Orban amepongeza uamuzi wa Ujerumani.Hungary iko kwenye mpango wa kujenga uzio katika mpaka wake na Serbia kwa lengo la kuwazuia wahamiaji.

Nchi hiyo itapitisha sheria mpya wiki ijayo itakayoruhusu kuwarudisha wahamiaji walipotoka iwapo wataingia nchini humo kinyume cha sheria.