Kiir aahidi kutekeleza mkataba wa amani

Salva Kiir
Image caption Kiir amesema yuko tayari kutekeleza kwa dhati mkataba wa amani

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amehutubu kupitia runinga ya taifa nchini humo na kusema amejitolea kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi uliopita.

Bw Kiir hata hivyo alikariri msimamo wake wa awali kwamba alitia saini mkataba huo akiwa na vifungu kadha ambavyo hakubaliani navyo.

Alitaja vifungu hivyo kuwa kile kinachotaka majeshi yaondolewe mji kuu wa Juba pamoja na kuteuliwa kwa mtu kutoka nje kufuatilia utekelezaji wa mkataba huo. Amesema huo ni “ukiukaji wa uhuru wa taifa.”

Kiongozi huyo ametoa hotuba hiyo kukiwa bado na shaka kuhusu kufanikiwa kwa mkataba huo kutokana na visa vya mara kwa mara vya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na mambo ambayo yeye mwenye hakubaliani nayo.

Bw Kiir alisema pia kuwa kuna watu “wanaojificha chini ya meza yetu” kwa lengo la kuvuruga mpango wa kurejesha Amani.

Rais huyo na kiongozi wa waasi nchini humo Riek Machar walitia saini mkataba huo wa amani baada ya shinikizo kutoka kwa viongozi wa kanda, Amerika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.