Turnbull aapishwa kuongoza Australia

Malcolm Turnbull
Image caption Turnbull amesema amejawa na matumaini kuhusu Australia

Malcolm Turnbull ameapishwa kuwa waziri mkuu mpya wa Australia baada ya kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa waziri mkuu Tony Abbott.

Kiongozi huyo mpya amesema huu ndio wakati bora zaidi wa kuwa raia wa Australia.

Bw Turnbull, aliyekuwa waziri wa mawasiliano katika serikali ya Abbott, sasa atakuwa waziri mkuu wa nne nchini humo tangu 2013.

“Nimejawa na matumaini tele na tutatulia katika wiki chache zijazo. Kwa miezi michache ijayo tutaweka msingi wa mambo yatakayotuwezesha kupata ufanisi katika miaka ijayo,” amesema.

Bw Abbott, aliyeondolewa mamlakani Jumatatu baada ya kura ya haraka kufanywa katika chama tawala cha Liberal, amesema aliondolewa kwa “uchungu” lakini ameahidi kurahisisha shughuli ya mpito kadiri anavyoweza.

Bw Turnbull anatarajiwa kukutana na wabunge wa chama cha Liberal na baadaye kukutana na wabunge wa muungano wa vyama vya Liberal na National vinavyotawala.

Anatarajiwa kutangaza baraza jipya la mawaziri kufikia mwisho wa wiki.