Wahamiaji wakwama mpakani

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Hungary imeweka kizuizi kikali dhidi ya wahamiaji

Mamia ya wahamiaji wako katika hali ya sintofahamu katika eneo la mpaka wa Serbia na Hungary baada ya Serikali ya Hungary kufunga mpaka wake kwa uzio.

Hatua hiyo inadhumuni la kuwazuia wahamiaji wanaojaribu kuingia katika nchi za jumuia ya Ulaya.

Baada ya sheria mpya nchini Hungary kuanza kufanya kazi, Polisi waliifunga reli iliyokuwa ikitumiwa na maelfu ya wahamiaji.

Baadhi wamekuwa wakitafuta namna ya kuuvuka uzio huo huku wengine wakirusha vyakula na maji kuonyesha kutofurahishwa na hatua ya Serikali ya Hungary.

Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo,Peter Szijjarto amesema nchi yake inapanga kujenga uzio katika eneo la mpaka wa nchi yake na Romania kuzuia wahamiaji.

Nchi za Umoja wa Ulaya zinakabiliwa na wimbi kubwa la wahamiaji, wengi wao wakikimbia migogoro na hali ya umasikini katika nchi zao ikiwemo Syria, ambapo kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2011.