Afrika Kusini yanyimwa rufaa kuhusu ICC

Omar al Bashir Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bashir pia alizuru Uchina wiki mbili zilizopita licha ya kuwepo kibali cha kumkamata

Mahakama nchini Afrika Kusini imeinyima serikali ya nchi hiyo ruhusa ya kukata rufaa uamuzi ulioishutumu kwa kukosa kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir alipohudhuria kongamano kuu la Muungano wa Afrika mjini Johannesburg mwezi Juni.

Serikali ilitaka kukata rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu ikisema Bashir alikuwa na kinga ya urais kwa sababu yeye ni kiongozi wa taifa.

Lakini Jaji Hans Fabricius amesema rufaa hiyo haiwezi kufanikisha chochote.

Ameongeza kuwa Afrika Kusini ni mwanachama wa Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo, na kwamba mkataba huo unabatilisha sheria zozote ambazo huenda zingempa kinga Bashir asikamatwe na kushtakiwa.

Kiongozi huyo wa Sudan amekuwa akisakwa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na makosa ya uhalifu wa kivita Darfur.

Kiongozi huyo aliyechukua mamlaka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 amekanusha madai hayo.