Boko Haram ‘wameua watu 380’ Cameroon

Wanajeshi wa Cameroon Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wa Cameroon wamo kwenye kikosi cha kanda kinachopambana na Boko Haram

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International limesema raia 380 wameuawa na wapiganaji wa Boko Haram kaskazini mwa Cameroon mwaka huu.

Ripoti iliyotolewa leo na shirika hilo inasema kuna wanajeshi kadha waliouawa na wapiganaji hao ambao wamelazimisha watu 80,000 kutoroka makwao.

Wanajeshi na polisi wa Cameroon nao wanadaiwa kujibu mashambulio ya kundi hilo kwa kuwakamata watu zaidi ya 1,000, wengi wao vijana.

Ripoti hiyo kwa jina "Cameroon human rights under fire", inasema baadhi ya waliokamatwa na maafisa wa usalama wameuawa au kufariki kutokana na hali mbaya gerezani, hasa katika mji wa Maroua.

Shirika hilo linasema watu 200 waliokamatwa na maafisa wa usalama kwenye operesheni Desemba kwa sasa hawajulikani waliko.

Amnesty wanaamini Cameroon inaweza kujifunza mengi kutokana na makosa yaliyofanywa na taifa jirani la Nigeria ambako wanajeshi wametuhumiwa kutekeleza dhuluma dhidi ya raia kwa muda mrefu.

Kundi hilo linasema yaliyotokea Nigeria yanaonyesha kukosa kuheshimu haki za kibinadamu na sheria za kimataifa kuhudu ubinadamu katika vita dhidi ya Boko Haram kuna madhara makubwa.

Katika kisa kimoja kaskazini mwa Cameroon, shirika hilo la haki za kibinadamu linasema maafisa wa usalama walishambulia shule za kutoa mafunzo ya Kiislamu ambazo waliamini zilikuwa kambi za mafunzo za Boko Haram.

Watoto 84 na wanaume zaidi ya 43, wakiwemo walimu wengi, walizuiliwa kwa miezi sita bila kufunguliwa mashtaka, shirika hilo linasema.

Katika visa vingine, wanajeshi wa Cameroon wanadaiwa kupora mali na kuteketeza nyumba za watu.