Facebook kuwa na kitufe cha 'Kutopenda’

Mark Zuckerberg Haki miliki ya picha AP
Image caption Zuckerberg hataki kitufe cha kutopenda kitumiwe kupuuzilia mbali watu au kueneza chuki

Mwanzilishi na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Facebook Mark Zuckerberg amesema mtandao huo utaongezwa kitufe chenye alama ya kuonyesha kutopendezwa na jambo.

Hatua hiyo inakusudia kuwewezesha watumiaji kuonyesha hisia zao kwa ufasaha.

Zuckerberg anasema kampuni imeombwa mara nyingi kutafuta njia mbadala ya kutumia kitufe cha kuonyesha kutopenda baadhi ya vitu vinavyopakia kwenye mtandao huo kama vile picha za ajali au vifo.

Anasema kitufe hicho kinaweza kutumika kuonyesha kusikitishwa na jambo fulani. Kwa sasa kitufe hicho kinaendelea kuboreshwa na karibuni kitaanza kufanyiwa majaribio.

“Mamia ya watu wameomba kuwe na kitufe hiki, na leo ni siku ya kipekee kwa sababu ninatangaza kwamba tunaandaa kitufe hiki, na tuko karibu kuanza kukifanyia majaribio,” alisema Zuckerberg akiongea katika makao makuu ya Facebook yaliyoko Menlo Park, California.

Hata hivyo amesema kitufe hicho kitumiwe na watu kupuuzilia mbali jumbe, picha au video za wengine au kuchukiza watu.

Badala yake, anataka kiwe kikitumiwa katika hali ambazo huwa si vyema kutumia kitufe cha ”kupenda” hasa kwenye jumbe za kuhuzunisha.

Kwa sasa, watumiaji wa mtandao huo wamekuwa na fursa ya kupenda tu, kitufe kilichoanza kutumiwa mwaka 2009.