Urusi yazuia vikwazo vya UN Sudan Kusini

Wapiganaji Sudan Kusini Haki miliki ya picha AFP
Image caption Angola inataka pande zote zipewe muda wa kutekeleza mkataba wa amani

Urusi na Angola zimepinga pendekezo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuwekea vikwazo afisa mkuu mmoja wa jeshi la Sudan Kusini na kamanda mmoja wa waasi, wanadiplomasia wamesema.

Baraza hilo lilitaka wawili hao waadhibiwe kwa mchango wao katika vita vilivyoendelea kwa miezi 20 sasa nchini humo.

“Marekani, mara nyingi husema tu ‘vikwazo, vikwazo, vikwazo’ na katika hali nyingine hili hata hufanya hali kuwa mbaya Zaidi,” balozi wa Urusi katika UN Vitaly Churkin alisema.

Watu karibu milioni nne wanakabiliwa na uhaba wa chakula Sudan Kusini.

Marekani ilikuwa imependekeza kwa kamati ya vikwazo ya Baraza la Usalama la UN kwamba mkuu wa jeshi la Sudan Kusini Paul Malong na kamanda wa waasi Johnson Olony wawekewe vikwazo vya kutosafiri na mali yao izuiwe.

Shirika la habari la Reuters linasema Venezuela iliungana na Urusi na Angola kuzuia kuidhinishwa kwa pendekezo hilo.

Wanadiplomasia wanasema Angola ilitaka pande zote mbili zipewe muda zaidi wa kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi uliopita.